NYAYO ZA KIDIGITALI
NYAYO ZA KIDIGITALI NI NINI?
Ulinganifu wa kawaida; ni nyayo unazoacha nyuma yako pale unapotembea kwenye ufukwe wa bahari — kila hatua unayopiga inaacha alama kwenye mchanga ambayo inaruhusu mtu mwingine kuona na kufuatilia alama hizo.
Tofauti na nyayo kwenye ufukwe wa bahari ambazo zinaweza kufifia au kupotea kabisa kutokana na mawimbi; mtandao na matukio ya kielektroniki kwa ujumla wake — haifanyi kazi hivyo. Ni salama kudhani kwamba chochote unachokifanya na unachochapisha mtandaoni kitakua hapo kwa kudumu na hakitafifia au kuondoka kabisa.
Taarifa unazozishiriki mtandaoni zinaweza kutumika kukuelezea wewe ni mtu wa aina gani pamoja na shughuli zako na vitu unavyopendelea. Ni muhimu kufikiri kwa kina kuhusu nani anapaswa kuona taarifa hizo, na kukumbuka kwamba hata kama umeweka vizuri sana mipangilio yako ya faragha (privacy settings), bado wengine wanaweza kusambaza zaidi maudhui uliyochapisha.
Kimsingi, inalipa sana kufikiri kabla hujaweka chochote mtandaoni. Mara unapoweka kitu mtandaoni, unapoteza udhibiti wa maudhui hayo; na yanaweza kusambazwa na kusababisha usumbufu mwingine ambao haukukusudiwa mwanzoni.
HATARI YAKE NI NINI?
Watu wengi wanatengeneza nyayo za kidigitali wanapotumia huduma mbali mbali za kimtandao.
Wanaweza kuchapisha taarifa zao wenyewe mfano; taarifa binafsi au picha kuhusu sherehe, au matukio mbali mbali yanayowahusu. Pia wanaweza kushiriki (na mara nyingi kwa kutokukusudia) kutengeneza ‘metadata’ kwa huduma wanazozitumia mtandaoni. Hii inaweza kuwa anwani ya kimtandao ya kifaa unachotumia (IP address), pamoja na mwenendo wa kuvinjari (browsing behaviour) na taarifa zingine za mtumiaji wa mtandao.
Baadhi ya hatari ambazo zimekuwa zikiripotiwa mara kwa mara ni;
1. Uchapishaji wa taarifa binafsi zinazopelekea uonevu na unyanyasaji kimtandao (cyber bullying).
2. Kuchapisha picha au video zinazotumika kwa maudhui ya kingono.
3. Kuchapisha taarifa za kibiashara zinazoweza kutumika kwa mashambulizi ya uhandisi jamii (social engineering attacks)
4. Kuchapisha taarifa zinazoweza kusababisha uharibifu wa sifa ya mtu (reputation) au hata kupoteza ajira.
NIFANYEJE KUHUSU NYAYO ZANGU ZA KIDIGITALI
Kwa kuanzia, tafuta jina lako kwenye mtandao na uone kinachotokea. Kuondoa maudhui inaweza kuwa ngumu, hivyo ni vizuri kufikiri kwa umakini sana kuhusu kila unachochapisha au kutuma mtandaoni.
Fikiri kwa kina kuhusu nani ataona maudhui hayo, na hasa kama yakisambaa kwa hadhira ambayo haikukusudiwa, familia, marafiki au hata waajiri. Pia jenga mazoea ya kutumia mipangilio ya faragha (privacy settings) kwenye mitandao na majukwaa (platforms) uliyopo.
NAMNA UNAVYOWEZA KULINDA NYAYO ZAKO ZA KIDIGITALI
Vipo vidokezo kadhaa unavyoweza kuzingatia ili kulinda nyayo zako za kidigitali;
1. Thamini sana taarifa zako binafsi.
2. Kuwa makini sana na kila unachochapisha mtandaoni.
3. Fikiri kuhusu faragha yako kimtandao (online privacy) pia hakiki mipangilio ya majukwaa uliyopo (platform settings)
4. Fanya tathmini ya kina ya athari za muda mrefu (kwako na kwa wanaokuzunguka) zinazoweza kusababishwa na picha, video au maoni utakayochapisha mtandaoni.
Mitandao salama inaanza na mimi.